Alhamisi , 9th Jul , 2020

Licha ya Serikali kuwa na mpango madhubuti wa kujenga uwanja mkuwa kwa ajili ya shughuli kubwa za michezo, mkufunzi wa timu za Taifa za vijana nchini Bahati Mgunda amesema mchakato huo ni mzuri ingawa umechelewa sana.

Mkufunzi wa timu za Taifa za vijana za mpira wa kikapu Tanzania Bahati Mgunda (pichani).

Akizungumza na kipindi cha michezo cha Kipenga, kinachorushwa kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 2 usiku, East Africa Radio, Mgunda amesema yeye binasfi amesafiri katika mataifa mengi ambayo yamenufaika sana na uwepo wa Arena.

Mgunda ameongeza kuwa suala hilo limekuja wakati muafaka,kwa kuwa Arena inafungua mambo mengi kimataifa, kutokana na uwezekano wa nchi kupewa uwenyeji wa mashindano mbali mbali ya kimataifa ambayo yanasaidia kuitangaza nchi na pia kuongeza uchumi wa nchi kupitia michezo.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa, amesema mwaka jana alisimamia mashindano ya vijana ambayo yalishirikisha nchi mbali mbali ambayo yalichangia kiasi cha milioni 30 kwa Taifa, hivyo anaamini itakuaje kama tutakua wenyeji wa mashindano ya wakubwa.

Aisha amewataka watanzania kuwa tayari kuipokea Arena hiyo namna ya kunufaika na uwanja huo mkubwa, ili kuithibitishia Serikali kwamba inahitajika kujenga viwanja kama hivyo katika mikoa mbali mbali ambayo itaukuza mchezo wa mpira wa kikapu lakini kuiingizia kipato nchi.

Ikumbukwe Serikali kupitia katibu wa wizara ya habari,utamaduni,sanaa na michezo, Dokta Hassan Abbas ilitoa ahadi ya kujenga Arena ndani ya miezi sita ijayo kuanzia ili kufanikisha kufanyika kwa mashindano na matukio makubwa ya michezo na burudani kama ambavyo Rwanda inavyonufaika hivi sasa.