Tanzania imefuzu hatua ya makundi, Kaseja aeleza

Jumapili , 8th Sep , 2019

Timu ya taifa ya Tanzania imesonga mbele kwenye hatua ya makundi, kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar mwaka 2022.

Juma Kaseja na Mbwana Samatta pamoja na mwamuzi wa mchezo.

Tanzania imefanikiwa kupata ushindi wa jumla kwenye mechi zote mbili dhidi ya Burundi, baada ya kushinda kwa penalti 3-0 baada ya mechi zote mbili kumalizika kwa sare ya 2-2.

Katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa taifa leo Septemba 8, 2019, Tanzania ilitangulia kwa goli la mapema dakika ya 29 kupitia kwa nahodha Mbwana Ally Samatta.

Burundi ilisawazisha kupitia kwa Abdul Razak dakika ya 45 kipindi cha kwanza hivyo kufanya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1 hivyo kwenda dakika 120 ambazo nazo zikamalizika kwa sare hiyo hiyo.

Katika mikwaju ya penalti Tanzania iliwakilishwa na Erasto Nyoni ambaye alifunga kisha Himid Mao pamoja na Gadiel Michael, ambao nao wakapata huku Burundi wakikosa zote ikiwemo penalti moja aliyoidaka Juma Kaseja.

Baada ya mchezo Kaseja amesema wachezaji wenzake wanafarijika kutokana na umoja wa mashabiki uliopo unawafanya wajitoe kwaajili ya taifa.

''Hiki kipaji cha kudaka penalti nadhani nimebarikiwa tu na Mungu, hakuna kocha aliyenifundisha kudaka penalti'', amesema.

Tanzania sasa inaungana na timu zingine kwaajili ya kukamilisha timu 40 za bara la Afrika zitakazopangwa kwenye makundi kwaajili ya kusaka nafasi tano za kuwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia.