Jumatatu , 13th Jun , 2016

Kiungo mkabaji wa timu ya Yanga Salum Telela ambaye amemaliza mkataba wake na baadaye kutoonekana katika timu hiyo ni kama amepotezewa baada ya uongozi wa klabu hiyo kutomzungumzia wakati wenzake wakiondoka nchini jumapili kuelekea nchini Uturuki.

Aliyekuwa kiungo mkabaji wa timu ya Yanga Salum Telela.

Salum Telela kiungo mwenye mapafu ya mbwa na mwenye uwezo wa kuzima na kujenga mashambulizi inasemekana hatokuwepo msimu ujao hii ni baada ya chanzo kimoja kutoka ndani ya klabu hiyo kusema kiungo huyo hana nafasi kufuatia mlundikano wa viungo bora wanaocheza nafasi hiyo na ambao wamekuwa ndiyo chaguo la kocha Mdachi (Pluijm).

Baadhi ya viungo ambao wamekuwa wakimpa wakati mgumu kiungo huyo chipukizi mwenye uzoefu na eneo la katikati ya kiwanja ni pamoja na raia wa Zimbabwe Thaban Kamusoko ambaye ndiye chaguo la kwanza la kocha Hans Van der Pluijm huku pia kwa wakati mwingine huwa anawatumia Mnyarwanda Mbuyu Twite na Chipukizi Mtanzani Juma Makapu na kwa nyakati tofauti amewahi pia kumchezesha katika nafasi ya kiungo beki wa kati wa timu hiyo raia wa Togo mwenye asili ya Ivory Coast Vicent Bosuou ambaye pia anaimudu vyema nafasi hiyo ya kiungo mkabaji.

Chanzo hicho ambacho hakikutaka kuwekwa hadharani kutokana na suala hilo bado liko jikoni kimeshangazwa na kukiri kuwa bado haijafahamika haswa sababu za Telela kutoongezewa Mkataba, licha ya umuhimu wake wa wazi unaoonekana katika timu kwa sababu ni kiraka anayeweza kucheza kama beki wa kulia, kati na nafasi zote za kiungo.

Chanzo hicho kilienda mbali zaidi na kugusia suala la nidhamu kwa mchezaji huyo kikijiuliza labda pengine ndiyo sababu ya mchezaji huyo kupotezewa na benchi la ufundi na uongozi wa timu hiyo?

Jibu likaja hapana kuhusu suala la nidhamu, Telela anaonekana ni mchezaji mwenye nidhamu, bidii ya mazoezi na kujituma, ambaye wakati wote anapoingizwa uwanjani licha ya muda mwingi kuwa mchezaji wa akiba hucheza vizuri kwa kufuata maelekezo na kutimiza wajibu na kutoa matokeo chanya kwa timu.

Kwa upande mwingine chanzo hicho kimesema uhenda kusajiliwa kwa kipa bora chipukizi Beno Kakolanya kutoka maafande wa Tanzania Prisons ya Mbeya ndiyo kumefungua mlango wa kutokea kwa kipa mwingine chipukizi mrefu Benedict Tinocco ambaye chanzo hicho kinasema huenda akatolewa kwa mkopo kama si kupewa mkono wa kwaheri.

Lakini Habari za ndani zinasema kipa Benedictor Tinocco atatolewa kwa mkopo, maamuzi hayo yamepitishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm.

“Tinocco atatolewa kwa mkopo sehemu ambayo anaweza kupata nafasi ya kucheza, ili kama atapandisha uwezo wake, anaweza kurudishwa.

Wakati huo huo, Yanga inaendelea kusubiri ofa ya kumuuza mshambuliaji wake Paul Nonga ambaye hivi karibuni aliuandikia barua uongozi wa klabu hiyo akiomba kuuzwa, ili kwenda timu ambayo atakuwa anacheza mara kwa mara.

Nonga aliyesajiliwa Desemba kwa dau la Sh. Milioni 20 kutoka Mwadui FC ya Shinyanga ameamua kuondoka baada ya kushindwa ushindani wa namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo mbele ya kundi la washambuliaji wenye viwango na vipenzi vya kocha Pluijm.

Washambuliaji chaguo la kwanza wa Yanga ni Mzimbabwe Donald Ndombo Ngoma na Mrundi, Amissi Tambwe wakati Nonga alikuwa wa akiba pamoja na Malimi Busungu na Matheo Anthony.

Na katika taarifa nyingine toka ndani ya Yanga zinasema tayari klabu hiyo imempa mkono wa kwaheri ama imeachana rasmi na kiungo kutoka Niger, Issoufou Boubacar ambaye pia alisajiliwa katika dirisha dogo mwezi Desemba mwaka jana.

Mpaka sasa Yanga imeshafanya usajili wa nyota wanne wa ndani huku ikiendelea na mawindo zaidi kwa wachezaji wengine kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia matakwa ama mahitaji ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Wachezaji ambao Yanga imewanasa mpaka sasa ni beki kisiki wa upande wa kulia Hassan Ramadhan 'kessy' waliyemtwaa kutoka klabu ya Simba ambako alimaliza mkataba wake.

Wengine ni pamoja na beki wa kati Vicent Andrew 'dante' ambaye ametokea kwa wakata miwa timu ya Mtibwa Sukari ya Morogoro, mwingine ni kiungo fundi wa wagosi wa kaya Coastal Union ya Tanga chipukizi Juma Mahadhi ambaye ni mjukuu wa kipa wa zamwani wa Simba na Taifa Stars Omar Mahadhi bin Jabir.

Na wanne ni kipa chipukizi wa Tanzania Prisons ya Mbeya Beno Kakolanya wote hao wanne ni wachezaji wa kiwango cha kimataifa na uzuri wameitwa katika kikosi cha timu ya Taifa iliyochini ya kocha mzawa Boniface Mkwasa na hata katika timu walizotoka walikuwa wako katika vikosi vya kwanza vya timu zao.