Jumatatu , 31st Jan , 2022

Timu soka ya Tanzania ya watu wanaoishi na Ulemavu ‘Tembo Warriors’ inataraji kuingia kambaini kuanzia mwezi ujao ili kujiandaa na michuano ya Kombe la Dunia linalotaraji kuanza Oktoba 1 hadi 9, 2022 Istanbul, Uturuki.

(Tembo Warriors dhidi ya Cameroon Disemba 1, 2021 mchezo uliowafanya wafuzu Kombe la Dunia baada ya ushindi wa 5-0)

Kuelekea kwenye michuano hiyo, Rais wa Shirikisho la Soka la Walemavu Nchini Tanzania ambao ndiyo walezi wa Tembo Warriors, Peter Sarungi amesema kwa sasa wanashukuru baada ya kujua tarehe ya michuano kwani inawasaidia kujipanga.

"Tunashukuru tarehe ya mashindano imetoka wakati ambao TAFF na Serikali tumeanza maandalizi ya timu yetu na sasa yamebaki mambo machache ili timu iingie kambini kuanzia mwezi ujao"

"TAFD imedhamiria kufanya vyema kwenye mashindano ya kombe la Duniani kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania na Soka la Walemavu" Alisema Sarungi.

Kwa upande mwingine, Sarungi amekiri kuwa Tembo Warriors ipo kwenye harakati za kumsajili Kocha  Mpya huku ikiwa kwenye mazungumzo na Nane Kwame ambaye alikuwa Kocha wa timu ya taifa ya Ghana na kuwapa Ubingwa wa CANAF.

Kwame pia ni kocha wa klabu ya Konye inayoshiriki Ligi kuu ya Walemavu Nchini Uturuki na Kocha mwingine ni Willis Odhiambo wa timu ya taifa ya Kenya.