Jumatatu , 23rd Jul , 2018

Ushindani uliooneshwa kwenye mechi ya robo fainali ya Sprite Bball Kings kati ya Temeke Heroes dhidi ya Portland, ulimgusa Rais wa shirikisho la mpira wa Kikapu nchini (TBF), Phares Magesa ambaye alikuwepo kwenye uwanja wa taifa wa ndani kushuhudia mechi hizo.

Timu za Temeke Heroes (jezi nyeupe) na Portland (kijani) kwenye mechi yao ya robo fainali.

Mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Portland kushinda kwa pointi 83 dhidi ya 70 za Temeke heroes ilishuhudiwa ikianza kwa ushindani mkubwa ambapo quater ya kwanza hadi ya tatu hazikuweza kutabiri mshindi hadi mechi ilipoingia quarter ya 4 ambapo Portland walijihakikishia kushinda.

Akifanya mahojiano maalum na www.eatv.tv baada ya mechi 4 za robo fainali, zilizofanyika kwenye uwanja wa ndani wa taifa, Magesa alisema mchezo wa Temeke heroes na Portland ni kivutio tosha cha mashabiki kuja uwanjani kwenye mechi zinazofuata kwani watakuwa wanaamini kuna burudani tofauti na timu zingepoteza kwa pointi nyingi.

''Kiukweli ushindani ni mkubwa sana. Mechi ya mwisho ilikuwa kama fainali huwezi kujua mshindi mpaka 'querter' ya mwisho. Vijana wameonesha viwango vikubwa sana na hiki ndio TBF tunataka ili mchezo huu uendelee kuwavutia mashabiki lazima ushindani wa aina hii uwepo'' - alisema.

Rais wa TBF Phares Magesa (kulia) akiwa na katibu wake Mike Mwita (kushoto) wakifuatilia mechi za robo fainali ya Sprite Bball Kings.

Magesa pia alitoa pongezi kwa waandaaji ambao ni East Africa Television LTD na wadhamini wa mashindano ambao ni kinywaji cha Sprite akisema huo ni mfano tu kwa wadau wengine kuona umuhimu wa mchezo huo na kujitokeza kuweka nguvu zao.

Bingwa wa michuano hii atajinyakulia kitita cha shilingi milioni 10 huku mshindi wa pili akitunza shilingi milioni 3 na mchezaji bora wa mashindano 'MVP' akihifadhi kiasi cha shilingi milioni 2. Droo ya mechi za nusu fainali leo, itaoneshwa moja kwa moja kwenye 5Sports na kusikika kupitia 'The Cruise'