Alhamisi , 12th Jul , 2018

Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kimemuondoa Clement Sanga aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB) kwenye nafasi hiyo, kwa kukosa sifa baada ya klabu ya Yanga kuthibitisha Yusuph Manji kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo.

Rais wa shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia

Hayo yameelezwa na Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Julai 12, 2018 na kusema kwamba kutokana na hilo Sanga amepoteza sifa ya kuwa kiongozi wa bodi hiyo kwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi anapaswa awe Mwenyekiti wa klabu inayoshiriki ligi kuu.

"Tulipokea barua Julai 12 kutoka klabu ya Yanga ikidai kuwa Sanga hatambuliki kama Mwenyekiti wa klabu hiyo, wao Yanga wanamtambua Yussuf Manji ndiye Mwenyekiti wa klabu hiyo na katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi unatakiwa uwe Mwenyekiti wa klabu yako", amesema Karia

Vile vile, Rais wa shirikisho hilo Wallace Karia, ameielekeza kamati ya uchaguzi ya Yanga kuandaa uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo.

Clement Sanga

Katika hatua nyingine, Karia amesema Kamati ya Utendaji imempitisha rasmi Wilfred Kidao kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kukaimu kwa muda mrefu.

Maamuzi hayo ya Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yamekuja  kufuatia mkutano uliofanywa Juni 10 wa wanachama wa Yanga na kusema bado wanamtambua Yussuf Manji kama Mwenyekiti wao.