Ijumaa , 11th Aug , 2017

Wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi mkuu TFF  wameongezewa nafasi ya mwisho kupiga kampeni zao ambapo wameruhusiwa mpaka kesho kabla ya upigaji kura kuanza watakuwa huru kuendelea na kampeni.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo, Wakili Revocatus Kuuli amewaambia  wagombea kuwa wapo huru kufanya kampeni zao hadi Jumamosi  asubuhi ambapo uchaguzi huo unategemewa kufanyika kwenye Ukumbi wa St Gasper mjini Dodoma na ajenda  kuu katika mkutano mkuu ikiwa ni uchaguzi mkuu pekee.

Awali Kamati ya Uchaguzi ilitangaza muda wa siku tano wa kufanya kampeni hizo ambapo zilipaswa kufungwa leo Ijumaa saa sita usiku.

"Kila kitu kinakwenda sawa kabisa, tumeruhusu kampeni zifanyike hadi kesho asubuhi kabla ya kuanza uchaguzi, kampeni hizo ni zile za chini chini na utulivu mkubwa ili zisiingiliane na ratiba nyingine. Tutakapoanza taratibu zingine kama kuhakiki hapo ndio zitafungwa rasmi, kikubwa narudia kuwaomba wagombea na wapiga kura kuzingatia umakini kwani sheria zipo wazi," alisema Kuuli.

Wagombea 65 wapo Dodoma  tangu Jumatano wakitengeneza mazingira kwa wapiga kura huku kila mgombea akionekana anapambana kuomba kura huku Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ikiwa imepiga kambi Dodoma kufuatilia mwenendo wa uchaguzi huo.