
Timu ya taifa ya Tanzania Taifa stars inashiriki fainali za CHAN kwa mara ya pili, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009
Jumla ya wachezaji 30 wameitwa kuunda kikosi cha Tanzania kitakachoingia kambini Januari 1, 2020, kujiandaa na fainali za CHAN zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani, lakini pia kikosi hicho cha Taifa Stars kitacheza michezo 2 ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya DR Congo kabla ya fainali hizo.
Baada ya kikosi hicho kutangazwa, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikiso la Mpira wa Miguu hapa Nchini TFF Oscar Milambo, alitolea ufafanuzi juu ya nini malengo ya shirikisho katika ushiriki wa Taifa stars kwenye fainali za CHAN, amesema malengo ni kuvuka hatua za juu ukilinganisha na ushiriki wetu wa mwisho kwenye mashindano hayo.
“CHAN tunaenda kucheza kwa mara ya pili tunayakumbuka vizuri matokeo ya awamu ya kwanza ambayo tulienda kucheza, lengo letu la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunaenda kufanya vizuri kwenye matokeo ambayo tulikuwa nayo mara ya mwisho, kama tuliishia kwenye hatua ya makundi, basi tuchukue kuanzia hapo halafu tuendelee kwenye hatua zinazofatia”, amesema Oscar Milambo.
Mara ya kwanza Tanzania ilishiriki fainali za michuano ya CHAN mwaka 2009, fainali ambazo zilifanyika Ivory Coast, ambazo zilikuwa fainali za kwanza za michuano hii, na Taifa Stars ilitolewa hatua ya makundi kwenye fainali hizo.
Tanzania ilipangwa kundi A sambamba na wenyeji Ivory Coast, Zambia na Senegal. Taifa stars ilimaliza nafasi ya 3 kwenye kundi hilo ikiwa na alama 4 baada ya kushinda mchezo 1, kutoka sare mchezo 1, na kufungwa mchezo 1.
Alipoulizwa kuhusu uteuzi wa kikosi ambacho kimekuwa kinakosolewa kutokana na baadhi ya wachezaji wanaonekana kuwa kwenye kiwango bora, kutojumuishwa kwenye kikosi hicho , Oscar amesema mwalimu ndio anapaswa kujibia hilo.