Jumatatu , 2nd Jul , 2018

Baada ya kufanyika kwa hatua ya kwanza ya mchujo ya Sprite Bball Kings wiki iliyopita, michuano hiyo itaendelea wiki hii ambapo droo yake itafanyika leo katika studio za EATV zilizopo Mikocheni Jijini Dar Es Salaam.

Timu zilizoshiriki hatua ya mchujo ambapo Dream Chaser waliovalia jezi nyeusi wakipambana na Temeke Heroes (nyeupe)

Jumla ya timu 15 zilizofuzu hatua ya kwanza ya mchujo wiki iliyopita zitaungana na bingwa wa mwaka uliopita Mchenga Bball Stars katika hatua ya 16 bora ambapo droo hiyo itaanza na semina majira ya saa 1:00 usiku na baadae kumalizia na droo.

Timu zilizofuzu ni The Team Kiza, Stylers, St.Joseph, Oysterbay, Flying Dribblers, Portland, Raptors, Ukonga Hitmen, Ukonga Warriors, Temeke Heroes, water Institute, Fast Heat, Mbezi Beach KKKT, Air Wings, DMI na mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars.

Michuano ya mwaka huu inaonesha kuwa na msisimko mkubwa kutoka kwa washiriki na wadau wa mchezo wa kikapu kwa ujumla na hiyo inadhihirika kutokana na namna ambavyo ushindani ulivyojitokeza katika hatua ya awali ambayo imepelekea timu ya TMT ambayo ilicheza fainali na Mchenga Bball Stars mwaka uliopita kuondolewa katika hatua ya mwanzo kabisa.

Katika hatua ya 16 bora, timu zote zilizofuzu zitapewa seti mbili za jezi kutoka kwa mdhamini wa mashindano hayo kinywaji cha Sprite pamoja na kulipiwa gharama za usafiri kutoka mahali ambako timu hizo zinatokea hadi Uwanjani.

Hatua ya awali ya mchujo ilishirikisha timu 50 ambazo zilicheza mchezo mmoja mmoja na kisha timu zilizoongoza kwa tofauti ya alama katika kila mchezo zikachaguliwa na kuunda timu 16 .