Jumatano , 8th Jan , 2020

Ili ukacheze Ulaya sio kitu rahisi, haswa ukiwa unatokea mataifa ambayo kwenye ramani ya soka hayapo hata kwenye nafasi 100 bora. Pongezi kwa Simon Msuva kutoka Yanga mpaka Difaâ Hassani El Jadidi na sasa anaelekea Panathinaikos ya Ugiriki.

Mbwana Samatta akiwa na Simon Msuva kwenye moja ya mechi za timu ya taifa.

Ili ufike Ulaya inabidi ukacheze ligi ambazo zinatazamwa zaidi na mawakala pamoja na Scouts wa vilabu vikubwa duniani. Kwa Afrika moja ya ligi hizo ni ya Afrika Kusini, Misri, Morocco, Cameroon, Nigeria, Ivory Coast, DR Congo na kwingineko ambako tayari wameshaliteka soko la Ulaya kwa kuwa na wachezaji wengi.

Msuva na Samatta nadhani walitafuta taarifa sahihi mapema, juu ya jinsi gani wanaweza kutimiza ndoto za kucheza Ulaya ama walifanyakazi na watu Smart na wakawapa njia za kupita ikiwemo kucheza ligi zinazofuatiliwa zaidi.

Leo ndoto zao zinazidi kutimia lakini wakiwa wamebeba mzigo mkubwa wa taifa.  Je kama wadau wa soka Mashabiki, Watangazaji, Wachambuzi na Mamlaka kama TFF, BMT, na Wizara  mpaka Serikali Kuu kwa Ujumla tunajua kama tunatakiwa kutumia hii fursa kuweka mazingira wezeshi kwa wengine kufuata nyayo hizi ?

Wakati mzuri ndio huu ambao bado Samatta na Msuva wanacheza ili utambulisho uwe rahisi kwamba natoka anapotokea mfungaji bora wa Mabingwa wa Ubelgiji KRC Genk au natokea anapotoka Winga wa Benfica ya Ureno anayecheza kwa mkopo Panathinaikos ya Ugiriki.

Endapo tutajisahau kutumia huu mlango uliopo wazi kwasasa, ukija kujifunga tutajuta. Kucheza Ulaya ukiwa unatokea Tanzania sio kazi rahisi kama tunavyodhani hata Wanyama alipotoka Tanzania alipita mataifa kadhaa ndio akafika White Hart Lane.

Kupitia kipindi cha Shabiki On Saturday kinachoruka kupitia East Africa Television, Msuva alikutana na Wanyama na alijikita kumuuliza namna ya kupenya na kuwavutia makocha wa Ulaya. Wanyama alimpa elimu nzuri siku hiyo na bila shaka ilimjenga kufika alipofika leo.

Tuungane tusaidie wengine wajipenyeze kwenye njia za kina Msuva na Samatta ili hii kazi iwe rahisi kadri miaka inavyokwenda. Hongera Simon Msuva kwa Deal hii, hakika umelifanya taifa liinuke.