''Tunakwenda kuchukua ushindi'' - Flying Dribblers

Ijumaa , 10th Aug , 2018

Kocha msaidizi wa timu ya Kikapu ya Flying Dribblers ambayo imetinga fainali ya michuano ya Sprite Bball Kings, Geoffrey Lea, amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Agosti 18 kwenye uwanja wa ndani wa taifa kwani wataondoka na ushindi dhidi ya Mchenga Bball Stars.

Flying Dribblers kwenye mechi yao ya game 2 nusu fainali dhidi ya Team Kiza.

Lea amesema timu yake inaendelea na mazoezi kwaajjili ya fainali ambayo wanakutana na mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars katika mechi 5 za fainali ambazo zitaamua timu gani inaondoka na kitita cha shilingi milioni 10 kwa bingwa na milioni 3 kwa mshindi wa pili.

''Tumeshajua tutacheza na nani kwahiyo tunachofanya ni kuandaa vizuri kikosi chetu ili tuanze kwa ushindi, kikubwa tu mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani sisi kama Flying Dribbllers hatutawaangusha'',- amesema.

Fainali ya Flying Dribblers na Mchenga ni kumbukumbu ya nusu fainali ya mwaka jana katika michuano hii inayoandaliwa na East Africa Television na kudhaminiwa na kiywaji cha Sprite. Katika nusu fainali hiyo Flying Dribblers ilitupwa nje ya mashindano na Mchenga kwenda fainali ambako walitwaa ubingwa.

Kocha msaidizi wa Flying Dribblers Geoffrey Lea kwenye mahojiano na East Africa Television.

Mechi za fainali zitaanza kupigwa Jumamosi Agosti 18 kwenye uwanja wa taifa wa ndani kabla ya mechi ya pili kupigwa Agosti 22 kwenye viwanja vya Don Bosco na game 3 itapigwa Agosti 25 uwanja wa ndani. Kama bingwa hatapatikana game 4 itapigwa Agosti 29 Don Bosco na game 5 itamalizika Septemba 1 uwanja wa ndani.