Ijumaa , 28th Dec , 2018

Afisa Habari wa klabu ya soka ya Yanga Dismas Ten amesema kuwa wana malengo ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ili iweze kufikisha mara 28.

Afisa Habari wa Yanga, Dismas Ten

Amesema hayo alipokuwa akizungumzia maandalizi ya mchezo wa Mbeya City dhidi ya Yanga ambao utapigwa Jumamosi katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

"Kama ambavyo mwalimu wetu amekuwa akisisitiza, lengo letu ni kushinda katika kila mchezo, tunahitaji kupata alama tatu. Tupo kwenye mbio za kutafuta ubingwa, tuliuazimisha msimu uliopita kwa hiyo mara hii tunahitaji kuurejesha Ili kuendelea kuandika rekodi ya kuchukua ubingwa Mara 28," amesema Dismas.

Kuhusiana na maandalizi ya mchezo huo, Ten amesema kuwa yanaendelea vizuri na kwamba kati ya wachezaji 20 ambao wamesafiri na timu hakuna ambaye anamajeraha yatakayomuweka nje ya mchezo.

"Asubuhi daktari amefanya vipimo kwa wachezaji wote na amesema kwamba katika wachezaji 20 waliokuja hakuna ambaye anatatizo kwa maana kwamba wote wapo vizuri na wana ari ya mchezo. Ni imani yetu kwamba tutapambana ndani ya dakika 90 kutafuta matokeo na kuifanya timu kupata alama tatu na kuzidi kuendelea kukaa kileleni," ameongeza.

Yanga inaelekea katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa msimu uliopita, ambapo ilipoteza kwa bao 1-0 .