Ufafanuzi wa Simba kuhusu kuwasimamisha mastaa

Jumatano , 9th Oct , 2019

Uongozi wa klabu ya Simba umefafanua juu ya tetesi za wachezaji wake Jonas Mkude, Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Clatous Chama zilizodai kuwa wachezaji hao wamesimamishwa.

Chama, Nyoni, Gadiel

Kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Simba ilifanya kikao cha ndani cha nidhamu mnamo Alhamisi, Oktoba 3 kujadili masuala ya kinidhamu pamoja na wachezaji hao kuhusu tuhuma za kutohudhuria mechi za kanda ya ziwa.

Klabu imesema kuwa kikao hicho kiliendeshwa kwa usawa na haki, ambapo walalamikiwa walitakiwa kujieleza na mashahidi waliitwa kutoa ushahidi kuhusiana na suala hilo.

Imesema suala hilo litamalizwa ndani ya klabu na kwamba kinachosubiriwa ni ripoti kutoka kwa kamati huru iliyoundwa na wanasheria wanne kuhakikisha kuwa haki inatendeka.

"Klabu ya Simba inasubiri wachezaji hao wamalize majukumu yao ya timu ya taifa kisha kukutana nao ili kulimaliza sakata hili, tofauti na taaria za uongo zilizotolewa kwenye baadhi ya vyombo vya habari mbalimbali kwamba wachezaji hao wamesimamishwa kwa kipindi cha mwezi mmoja kufanya shughuli zozote za klabu", imesema sehemu ya taarifa hiyo.