Jumamosi , 16th Jun , 2018

Zoezi la usaili wa timu zitakazoshiriki mashindano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings 2018, umekamilika jioni hii ambapo jumla ya timu 50 zimejiandikisha kushiriki michuano hiyo.

Usaili huo ambao umefanyika Mlimani City Mall kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni, umefanyika vizuri ambapo timu mbalimbali wakiwemo mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars zimejitokeza kujiandikisha.

Mbali na Mchenga pia mshindi wa pili wa michuano hiyo msimu uliopita TMT, nayo imejiandikisha tayari kwa kuusaka ubingwa wa msimu huu baada ya kuukosa msimu uliopita.

Katika uzinduzi huo pia timu ambazo zilishiriki mwaka jana na kuishia hatua ya mchujo, kama Portland na The Snipers zimejitokeza na kuahidi kufanya maandalizi mazuri msimu huu ili ziweze kufika hatua za juu zaidi.