Jumapili , 8th Mar , 2020

Leo majira ya jioni nchi itasimama kwa dakika 90 kupisha pambano la nguvu na la kihistoria katika ardhi ya Tanzania, ambapo vigogo Yanga na Simba watakapopambana katika mchezo wa Ligi Kuu.

Mchezo wa watani, Yanga na Simba

Timu hizi zimekuwa kubwa kiasi cha kukusanya mashabiki karibia robo tatu ya mashabiki wote wa soka hapa nchini, ambapo timu hizi zinapokutana huvuta hisia kubwa miongoni mwa wadau wa soka.

Tangu Machi 2015, timu hizo zimekutana mara 10, Yanga ikishinda mara moja pekee, zikienda sare mechi nne na mechi tano Yanga ikifungwa.

Mechi ya Yanga na Simba kawaida huwa ni mechi ngumu bila kuangalia nani yuko vizuri kwa kipindi hicho. Hiyo inajidhihirisha katika mchezo uliopigwa Disemba 20, 2013 ambao timu hizo zilitoka sare ya 3-3, Yanga ambayo ilikuwa bora ndani ya uwanja na nje ya uwanja chini ya tajiri Yussuf Manji.

Mechi nyingine ya mfano ni ile ya kwanza msimu huu ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, Yanga ikiwa haipewi nafasi au matarajio yoyote ya kushinda mchezo huo lakini mwisho ukamalizika kwa sare.