Jumatatu , 13th Mei , 2019

Kuelekea mchezo wa Ligi kuu soka Tanzania bara kati ya Simba SC dhidi ya Azam FC leo Mei 13, 2019, timu hizo zinatawaliwa na rekodi mbalimbali lakini kubwa ni katika mechi za ligi kuu.

Kushoto ni John Bocco na kulia ni Salum Abubakar Sure Boys

Timu hizo zimekutana mara 30 katika michuano yote hivyo leo itakuwa ni mechi au vita ya 31 kwao, ambayo pia inaweza kuamua mbio za ubingwa kwa Simba endapo watashinda.

Katika ligi kuu timu hizo zinakutana kwa mara ya 21 ambapo mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 4, 2008, Azam wakiwa wamepanda daraja lakini walishinda magoli 2-0 yaliyofungwa na Jamal Mnyate na Shekhan Rashid.

Katika mechi 20 zilizopita za ligi kuu, Simba wanaongoza kwa kushinda mechi 10 huku Azam FC wakishinda mechi 5 pekee na kutoka sara mara 5. Kwa ujumla zimekutana mara 30 ambapo Simba wameshinda mara 13 na Azam mara 12 huku zikitoka sare mara 5.

Tofauti kubwa katika mchezo wa leo ni kwamba wachezaji John Bocco na Salum Abubakar maarufu (Sure Boy), ndio wachezaji pekee waliokuwepo kwenye mechi ya kwanza mwaka 2008 na leo Bocco yupo Simba wakati Sure Boy bado yupo Azam FC.

Mechi inachezwa leo kwenye uwanja wa Uhuru Dar es salaam ambapo Simba ni mwenyeji. Itaanza saa 10:00 jioni. Simba ina pointi 81 kileleni wakati Azam FC ina pointi 68 katika nafasi ya 3.