Jumatatu , 4th Jul , 2016

Ule mzizi wa fitna juu ya nani atacheza fainali ya michuano ya Euro 2016 inayoendelea nchini Ufaransa itakatwa Julai 6 na 7 mwaka huu baada ya kupigwa kwa michezo miwili ya hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo michezo itakayanza saa 4 usiku.

Ratiba ya nusu fainali Euro 2016.

Michezo ya hatua ya nusufainali ya michuano ya kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2016 inayoendelea nchini Ufaransa inataraji kuanza kutimua vumbi kwa siku mbili kuanzia Julai 6 hadi 7 mwaka huu, ambapo mchezo wa nusu fainali ya kwanza Julai 6 utazikutanisha nchi za Ureno na Wales ambazo zote zinaongozwa na manahodha wake wachezaji tegemeo wa klabu bingwa ya Ulaya timu ya Real Madrid ya Hispania.

Nahodha wa Ureno ambayo imepenya katika hatua hiyo kwa bahati kutokana na mwendo wa kusuasua iliyoanza nao ni Cristiano Ronaldo ambaye ni mshambuliaji hatari na tegemeo wa Real Madrid huku kwa upande wa Wales ambao tangu kuanza kwa michuano hiyo wamekuwa wakicheza soka safi wao wanaongozwa na mshambulaji mwenye kasi na fundi wa mipira iliyokufa [free kick] Gareth Bale na wawili hao wanataraji kuonyeshana ubora wao na kurejesha upinzani wao wa nani zaidi na ataisaidiaje nchi yake.

Kwa upande wa nusu fainali ya pili ambayo itapigwa Julai 7 mwaka huu kati ya wenyeji Ufaransa watakapovaana na timu ngumu ya Ujerumani ambao ni mabingwa wa dunia na hii itakuwa mechi ya aina yake hasa ikizingatiwa inazikutanisha timu ambazo zina nyota wengi wanaotamba katika soka barani Ulaya lakini pia Ufaransa wao wakitaka kuendelea kutwaa makombe makubwa katika ardhi ya nyumbani mbele ya mashabiki wao huku Ujerumani maarufu kama mashine wao wakitaka kuweka rekodi kama ya Ufaransa yakutwaa kombe la dunia na baadae la Euro.

Hivyo kiufupi michezo hiyo yote ya nusu fainali hizo za Julai 6 na 7 itakuwa ni migumu mno na isiyotabirika na kimsingi lolote linaweza kutokea katika mechi hizo kuelekea kupata wanafinali wawili watakaovaana Julai 10 katika fainali itakayochukuwa nafasi katika dimba la Stade de Fance.

Katika michuano hiyo ya msimu huu imeshuhudiwa rekodi ya mabao ambapo nchi ya Wales ambayo imetinga hatua ya nusu fainali imekuwa ndiyo timu ya kwanza kufunga mabao mengi mpaka inaingia nusu fainali hiyo ikipasia nyavu mara 10 huku rekodi nyingine ikiwekwa na nchi ya Ukrain ambayo ilitolewa katika hatua ya makundi ikiwa timu pekee ambayo haikufanikiwa kupata bao hata moja.

Rekodi nyingine kwa mashabiki ilikuwa ni kufurika viwanjani ambapo kabla ya mchezo wa jana wa robo fainali kati ya wenyeji Ufaransa dhidi ya Iceland ushabiki ulionyesha kuwa zaidi ya mashabiki takribani milioni 2,154,900 walijitokeza kutazama mechi mbalimbali za michuano hiyo kuanzia hatua ya makundi, hatua ya 16 bora na mpaka robo fainali zilizopita kabla ya ile ya jana.

Lakini pia rekodi nyingine ya mashabiki kiwanjani iliwekwa katika mchezo baina ya Hispania na Italia ambapo mashabiki wachache zaidi kama 28,000 ndiyo walijitokeza uwanjani kutazama mtanange huo.

Michuano hii pia imetumika kuwatangaza wachezaji na sasa tutaanza kukona wakienda huku na kule, kwa mfano mshambuliaji Hal Robson Kanu wa Wales ambaye ameachwa huru na Reading mwishoni mwa msimu wa 2015-16 hivi sasa ameanza kutakiwa huku na kule na hasa baada ya bao lake lile alilogeuka katika kumi na nane akawabamiza Ubelgiji na kuipeleka Wales nusu fainali.