Jumatatu , 18th Jun , 2018

Mkali wa Hip Hop Bongo Wakazi, ambaye ni mdau mkubwa wa mpira wa Kikapu pamoja na michuano ya Sprite Bball Kings, amesema kwenye michuano ya mwaka huu inayoanza Juni 23 kwenye hatua ya mchujo hataishabikia tena timu hiyo.

Wakazi amefunguka hayo kwenye mahojiano na East Africa Radio, wakati wa usaili wa timu zitakazoshiriki michuano hiyo mwaka huu uliofanyika Jumamosi iliyopita Mlimani City Mall huku akieleza sababu kubwa ni yeye kutopenda timu zenye majina makubwa.

''Msimu huu siwaungi mkono tena Mchenga Bball Stars kwasababu wameshakuwa timu kubwa na mimi napenda timu ndogo zisizopewa nafasi mara nyingi huwa zinakuwa na vipaji vikubwa na huwa wanajituma sana ili kuonesha uwezo wao kwa wanaowabeza'', alisema.

Aidha Wakazi ameeleza kuwa atachagua timu mashindano yakianza kwani atakuwepo hivyo atajionea vipaji halisi na ataamua ashabikie timu gani kwenye msimu huu wa Sprite Bball Kings.

Kwa mujibu wa kamati ya michuano hiyo, mechi za hatua ya mchujo kwaajili ya kutafuta zile timu 15 zitakazoungana na bingwa mtetezi Mchenga Bball Stars zitaanza kupigwa Juni 23 hivyo wadau wa mchezo huo wajiandae kwaajili ya uzinduzi na mechi zenyewe.