Walichozungumza makocha na manahodha Simba, Yanga

Ijumaa , 3rd Jan , 2020

Kuelekea mchezo wa 'Watani wa Jadi' Simba na Yanga kesho Januari 4, leo umefanyika mkutano wa makocha pamoja na manahodha wa timu zote mbili kuelezea maandalizi yao.

Mkutano wa Simba, Yanga na wanahabari kuelekea mechi yao

Vifuatavyo ni baadhi ya vitu muhimu walivyovizungumza kuelekea kwenye mchezo huo.

Kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck amesema, "tumecheza mechi nne ndani ya siku 10 na tumeshinda zote, tunajua kuna hisia fulani unaweza kujihisi ni bora lakini hii ni derby na ina ugumu wake, ina hisia zake. Mitandaoni joto ni kubwa sana na kuna wanaosafiri mbali kuja kuitazama mechi hii pekee, hivyo tunajiandaa. Kikosi changu kipo vizuri isipokuwa Rashid Juma ambaye atakuwa nje wiki kadhaa lakini wengine wote wako fiti", amesema Sven.

Kocha wa Yanga, Boniface Mkwasa

"Tumetoka kwenye ratiba ngumu ya mechi lakini nashukuru tumepambana japo tumepata majeraha. Tumejiandaa vizuri kwa mchezo, kama wao wameshinda mechi nne tano basi na sisi tutakuwa wa kwanza kuwafunga", amesema Mkwasa.

"Tunawaheshimu Simba na katika mpira kila mmoja anajiandaa. Tunawaheshimu na wana uongozi na wachezaji wazuri lakini uwanjani maamuzi ni dakika 90. Tunawaomba waamuzi wachezeshe kwa uhalali bila shinikizo lolote", ameongeza.

Kuhusiana na majeraha ya timu yake, kocha Mkwasa amesema, "tutawakosa wachezaji wawili, Lamine Moro ambaye ana kadi tatu za njano na Tariq Seif ambaye aliumia katika mechi ya mwisho lakini wengine wote wako vizuri. Kila mchezaji wetu anataka kucheza hii mechi hata kama ni leo" 

Nahodha wa Simba, John Bocco amezungumzia kwa upande wao jinsi walivyojiandaa, "wachezaji tumejiandaa vizuri, tunajua ubora wa Yanga wana kocha na wachezaji wazuri. Tunaamini tutapata ushindi kesho kutokana na maandalizi tuliyopewa na kocha, pia matokeo ya mechi zetu hivi karibuni yanatupa morali" 

Naye nahodha wa Yanga, Juma Abdul kwa niaba ya wachezaji wenzake, amesema, "nawaomba mashabiki wetu wa Yanga wasiogope kitu wajitokeze kwa wingi kesho wakijiamini kwa sababu tumejiandaa kushinda. Mashabiki wa Simba wasije uwanjani na matokeo yao, yoyote aliyejipanga anataondoka na pointi tatu".