Jumatatu , 6th Aug , 2018

Baada ya kuishia hatua ya nusu fainali mwaka uliopita, timu ya Flying Dribblers, mwaka huu imekuwa timu ya kwanza kutinga fainali ya michuano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings baada ya kushinda mechi zao mbili kwenye 'best of three' za nusu fainali dhidi ya Team Kiza.

Timu ya Flying Dribblers wenye jezi nyeusi kwenye mchezo wao wa game 2 dhidi ya Team Kiza (nyeupe).

Safari ya Flying Dribblers kwenda fainali ilianza kwenye hatua ya mchujo ambapo ilicheza na timu ya Kurasini Worriors na kushinda kwa pointi 37 kwa 9. Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa JK Park, mchezaji Habirmana Mayeye alifunga pointi 11.

Baada ya kushinda mchujo, timu ya Flying Deribblers ilitinga 16 bora na kucheza na Ukonga Hitman kwenye uwanja wa Air Wing Ukonga ambapo ilishinda kwa pointi 87 kwa 63 na kutinga robo fainali. Katika mchezo huo mchezaji Baraka Mopele alikuwa kinara kwa kufunga pointi 36.

Kwenye robo fainali Flying Dribblers walicheza na Water Institute kwenye uwanja wa Bandari Kurasini ambapo walishinda kwa pointi 100 kwa 64, hivyo kujikatia tiketi ya nusu fainali. Katika mchezo huo Baraka Mopele alikuwa nyota kwa kufunga pointi 25.

Katika nusu fainali ambayo imechezwa kwa mtindo wa 'best of three' Flying Dribblers imeshuhudiwa ikimaliza kazi mapema tu baada ya kushinda 'game 1' na 'game 2' hivyo kuepuka kwenda 'game 3' dhidi ya wapinzani wao Team Kiza.

Flying Dribblers walishinda 'game 1' kwa pointi  84 kwa 70 za Team Kiza ambapo mchezaji Habirmana Mayeye alikuwa kinara kwa kufunga pointi 26, Assist 1 na rebound 4. Katika game 2 iliyopigwa Jumamosi Agosti 4 Flying Dribblers wakashinda tena kwa pointi 69 kwa 63 mara hii Baraka Mopele akifunga pointi 21 rebound 3 na Assist 1.

Flying Dribblers sasa tayari wameshajihakikishia milioni 3 kati ya 15 zinazotolewa kama zawadi na wadhamini ambao ni kinywaji cha Sprite ambapo bingwa ataondoka na milioni 10, milioni 3 kwa makamu bingwa na milioni 2 kwa mchezaji bora MVP. 

Flying Dribblers watajua mpinzani wao wa fainali siku ya Jumatano Agosti 8 ambapo Mchenga Bball Stars watacheza na Portland kwenye game 3 baada ya game 1 na game 2 kumalizika kwa kila timu kushinda mechi moja.