Baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu ya soka ya Simba wakiwa na mabango makao makuu ya klabu hiyo.
Uongozi na wachezaji wa timu ya soka ya wekundu wa Msimbazi Simba wametakiwa kujitathmini mwenendo wao mapema kabla hali haijawa mbaya ndani ya klabu hiyo kufuatia timu hiyo kuboronga katika michezo miwili mfululizo tena ikiwa nyumbani katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya mashabiki na wanachama wa timu hiyo hii leo wakati wakizungumzia hali ya kushtusha iliyoanza kujitokeza ndani ya klabu hiyo mara baada ya kujikuta ikipokea vipigo viwili mfululizo katika michuano mbalimbali inayoshiriki nchini.
Kadhia ya kwanza kwa wanachama na mashabiki hao wa Simba ilianza mara baada ya timu hiyo kutolewa na Coastal Union katika robo fainali ya kombe la FA ambayo mshindi wake atashiriki michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika hivyo hali hiyo ikafanya Simba kupoteza nafasi hiyo wanayoisaka bila mafanikio kwa mwaka wa tatu sasa.
Aidha kadhia ya pili ni hapo jana katika mchezo muhimu wa ligi kuu timu hiyo iliwasononesha wanachama hao baada ya kufungwa na Toto Africans kwa bao 1-0 na kusababisha tafrani kubwa kutokea kwa mashabiki wakiwashutumu viongozi kwa matokeo hayo mfululizo jambo lililosababisha askari wa usalama kuingilia kati na kuwatawanya mashabiki hao kwa mabomu ya machozi.
Wanachama hao wa Simba wakiwa na huzuni na jazba kubwa wamesema kwa mwanendo waliokuwa nao mwanzo kabla ya timu hiyo kusimama kucheza ili kupisha Yanga na Azam zimalize mechi zao za viporo wakilinganisha na sasa wanasema ni wazi kuna tatizo ndani ya uongozi wenyewe kwa wenyewe na pia hata wachezaji wameonesha kutokuwa na uchungu na timu.
Aidha wanachama hao wakaenda mbali zaidi na kusema pamoja na maneno maneno ya chinichini kuwa kuna mpasuko ndani ya uongozi wa timu hiyo sambamba na mgomo baridi wa wachezaji wakidai kuna mkono wa wapinzani wa timu hiyo wanaofukuzia nao ubingwa.