Ijumaa , 22nd Mei , 2020

Baada ya Rais Magufuli hapo jana Mei 21 kuruhusu kuruhusu michezo kuendelea, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imeruhusu klabu za soka kuanza kufanya mazoezi.

Wachezaji na benchi la ufundi wakiwa mazoezini

Akizungumza kuhusu utaratibu na muongozo utakaotumika kurejesha Ligi Kuu Tanzania Bara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbas amesema kuwa klabu za soka zinaruhusiwa kuanza mazoezi wakizingatia taratibu zote za kiafya pamoja na kutoruhusu mikusanyiko ya mashabiki.

"Wote tumefarijika kwa michezo kurejeshwa, kuna tahadhari za kuzingatia kutoka kwa Wizara ya Afya na TFF hasa ukizingatia kuwa ugonjwa upo ingawa unapungua sana, kwahiyo tahadhari mbalimbali zitatolewa na serikali na TFF", amesema Dkt. Abbas

"Kuanzia sasa ni ruksa kwa vilabu kufanya mazoezi, cha muhimu ni kwamba Wizara ya Afya ilishatoa maelekezo hasa suala la mikusanyiko. Kuhusu suala la mashabiki kwamba watakuwepo au hawatakuwepo ndio litaanza kujadiliwa", ameongeza.

Dkt. Hassan Abbas amesema klabu vianze mazoezi lakini viepuke mikusanyiko ya mashabiki na wachezaji na benchi la ufundi wazingatie maelekezo ya kiafya ikiwemo kunawa na kutumia sanitizer pamoja na kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu.