Alhamisi , 13th Aug , 2020

Klabu ya Namungo Fc ya Mkoani Lindi imemtambulisha kiungo Abdulhalim Humud kuwa mchezaji wake baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Kiungo AbdulhalimHumud akisaini mkataba wa kuitumikia Namungo Fc.

Humud amejiunga na Namungo akitokea Mtibwa Sugar aliyoitumikia hadi mkataba wake unamalizika na sasa anazima uvumi ulioenea kuwa huenda akijiunga na Klabu ya Yanga ya Jijini Dar es salaam.

Nyota huyo ambaye alikua na kiwango bora msimu uliomalizika, aliwahi kuvichezea vilabu vya Azam na Simba na hata KMC pia alicheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kwa nyakati tofauti.

Aliwahi kunukuliwa akisema kuwa yupo tayari kujiunga na Timu yoyote ikiwemo Mbao, Azam lakini kamwe hatoichezea klabu ya Simba huku akikataa kutoa maoni yoyote iwapo Yanga ingemuhitaji.

Ikumbukwe Namungo itaiwakilisha Nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika hivyo inafanya usajili wa kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya kufanya vyema katika michuano hiyo.