Jumamosi , 23rd Jun , 2018

Klabu ya soka ya Yanga, inatarajia kurejea kambini kesho Juni 24, 2018 tayari kwa kuanza maandalizi ya mechi zake za Kombe la Shirikisho Barani Africa katika hatua ya Makundi.

Viongozi wa nyadhifa mbalimbali ndani ya Yanga wakiwa na msemaji wa timu hiyo Dismas Ten (katikati) katika ofisi za timu hiyo.

Hilo limewekwa wazi na meneja wa timu hiyo Hafidh Saleh, ambaye amesema baada ya likizo waliyopewa wachezaji sasa ni wakati wa kurejea na kuanza kambi hivyo kuanzia kesho wachezaji watakuwa kambini.

''Yanga mipango yetu iko vizuri, tuliwapa likizo wachezaji na imemalizika hivyo kesho tunarejea rasmi na kuanza kambi kwaajili ya mechi yetu dhidi ya Gor Mahia itakayopigwa huko Kenya kati ya Julai 17 na 18'', amesema.

Yanga ina alama moja kwenye Kundi D, ambalo lina timu za USM Alger ya Algeria yenye alama 4, Rayon Sports ya Rwanda yenye alama 2 sawa na Gor Mahia ya Kenya.

Tayari Yanga imeshacheza mechi mbili za Kundi D na kuambulia kichapo kimoja cha 4-0 kutoka kwa USM Alger ugenini na kutoka sare na Rayon Sports kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.