Jumamosi , 14th Mar , 2015

Baada ya kufanikiwa kuvuka katika hatua ya kwanza ya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika Yanga Jumapili hii March 15 mwaka huu itakuwa na kibarua kingine cha mchezo wa kwanza wa raundi ya pili dhidi ya Wazimbabwe.

Kikosi cha wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika timu ya Yanga SC.

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa barani Afrika timu ya soka ya Yanga inataraji kutupa karata yake ya kwanza Jumapili hii katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam itakapopambana na timu ngumu ya soka ya Platnum ya Zimbambwe katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya kombe la shirikisho

Mjumbe wa sekretarieti ya timu hiyo Omary Kaya ameiambia muhtasari wa michezo kuwa kikosi kiko sawasawa na wamejipanga kuibuka na ushindi mkubwa kwakuwa tayari wanajua uzuri wa wapinzani wao baada ya kuwasoma na hivyo kufahamu vizuri mbinu zao kimchezo kitu ambacho kitawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha malengo yao ya kupata ushindi mkubwa ambao utawarahisishia kazi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa baada ya wiki mbili huko nchini Zimbabwe.