Jumatano , 29th Sep , 2021

Ligi kuu soka Tanzania Bara inataraji kuendelea tena jioni ya leo kwa michezo miwili, Maafande timu ya Polisi Tanzania watacheza na wakusanya mapato wa Halmashauri ya Kinondoni ‘KMC’ kwenye uwanja wa Karatu jijini Arusha wakati Kagera Sukari itawakaribisha Yanga kwenye dimba la Kaitaba.

Nahodha na beki kitasa wa klabu ya Yanga, Bakari Mwamnyeto atakayekosekana kwenye mchezo wa jioni ya leo kuptokana na maumivu ya kidole yanayomsumbua.

Kuelekea kwenye mchezo wa Yanga utakaochezwa saa 10:00 jioni, Afisa Msemaji wa Yanga, Haji Manara amethibitisha kuwa watamkosa nahodha wake beki kitasa, Bakari Mwanyeto ‘Nondo’ baada ya nyota huyo kuwa na maumivu ya kidole.

Kwa upande wa Makocha, Kocha wa wenyeji wa mchezo huo, Mkenya Francis Baraza amesema licha ya ukweli kuwa Yanga ni timu kubwa nchini lakini watacheza kwa kuwaheshimu na sio kuwaogopa ili wapate ushindi nyumbani.

"Tunataka kutumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani kwa kuanza na ushindi, hilo linaweselana kutokana na namna tulivyojiandaa na tumewaona wapinzani wetu usajili walioufanya na mbinu zao. Tutatumia upungufu wao kuwaadhibu"

Naye kocha wa Yanga, Mtunisia Mohammed Nasreddine Nabi amesema anatambua mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na Kagera Sukari kuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani lakini lazima wasake alama tatu muhimu.

“Hautakuwa mchezo rahisihasa kwa kuzingatia Kagera Sukari watakuwa nyumbani, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu kwetu kushindwa kupamaban kupata matokeo” Alisema kocha Nabi.

Mchezo huo ambao ni wa mwanzo wa Ligi kwa wawili hao utakuwa wa 23 kwenye Ligi Kuu pekee tokea Septemba 23, 2010 ambapo wawili hao wamecheza michezo 22, Yanga ikishinda michezo 17 na Kagera Sukari kushinda michezo 4 pekee.