Ijumaa , 5th Feb , 2021

Vinara wa Ligi kuu bara, klabu ya Yanga inataraji kucheza mchezo wa kirafiki Jumamosi ya kesho Februari 6, 2021 dhidi ya vinara wa kundi A wa Ligi daraja la kwanza, klabu ya African Sports ya jijini Tanga saa 1:00 usiku katika dimba la Chamazi jijini Dar Salaam.

Kikosi cha klabu ya Yanga, kilichoshiriki michuano ya kombe la Mapinduzi mwaka 2021.

Akizungumza na Kipenga Extra cha East Africa redio, Afisa mhamasishaji na msemaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema mchezo huo umelanga kuwapa utimamu wa mwili wachezaji kuelekea kwenye michezo ya ungwe ya pili ya Ligi kuu bara Februari 13, 2021.

Nugaz amethibitisha Yanga itawakosa washambuliaji wake tegemezi Said Ntibazonkiza na Yacouba Sogne ambao wanasumbuliwa na majeraha lakini kiungo Mapinduzi Balama ataendelea kukosekana kwa takribani majuma 3 licha ya kuwa upasuaji wake ulienda vizuri.

Amewataka mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kutaza burudani hiyo ya vinara hao ambayo itapambwa na uwepo wa wachezaji wapya ambao wamesajili kwenye dirisha hili dogo la usajili, mshambuliaji Fiston Abdul Razak na mlinzi wa kati Dickson Job.

Mchezo wa Yanga dhidi ya African Sports, utakuwa ni mchezo wa kwanza wa kirafiki wa Yanga tokea Januari 12 walipofanikiwa kubeba kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar baada ya kuwafunga watani wao wa jadi Simba kwa mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalty.

Yanga ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo ligi kuu bara wakiwa na alama 44, alama 6 mbele ya watani wao wa jadi Simba ambao wapo michezo miwili nyuma ya vinara hao, ilhali African Sports wanaongoza kundi A FDL kwa kuwa na alama 20 baada ya michezo 9.