Jumanne , 17th Jul , 2018

Klabu ya soka ya Yanga imeweka wazi kuwa wachezaji Kelvin Yondani na Hassan Kessy hawana mkataba na timu hiyo, ndio maana hawajasafiri na timu kwenda nchini Kenya kwaajili ya mechi ya kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Gor Mahia lakini hilo haliwatii shaka.

Kushoto ni Hassan Kessy na kulia ni Kelvin Yondani

Msemaji wa Yanga Dismas Ten alipoulizwa na www.eatv.tv juu ya hali ya kambi ya timu hiyo nchini Kenya na kukosekana kwa wachezaji Kelvin Yondani na Hassan Kessy ameeleza, timu iko kwenye hali nzuri lakini suala la Yondani na Kessy halina jinsi kwasababu hawana mkataba nao.

''Mikataba ya Yondani na Kessy imekwisha na bado hawajafikia makubaliano na kamati ya usajili ndio maana hawapo kwenye kikosi kilichokwenda Kenya wala sio sababu nyingine lakini waliopo wanatosha kuiwakilisha timu na ikarudi na matokeo mazuri'', - amesema.

Aidha Ten amefafanua kuwa sio kweli kwamba wachezaji hao wamegoma kama ambavyo imekuwa ikielezwa huko mitandaoni ni suala la mikataba tu ambalo kamati ya usajili inalifanyia kazi kama watafikia makubaliano watatoa taarifa.

Yondani na Kessy walisajiliwa na Yanga kutoka klabu ya Simba kwa nyakati tofauti akianza Yondani Julai 2012 na kisha Kessy Mei 2016. Yanga kesho itashuka dimbani kucheza na Gor Mahia kwenye mchezo wao wa tatu katika kundi D, baada ya kufungwa 4-0 na USM Alger kwenye mechi ya kwanza na kutoka sare ya 1-1 na Rayon Sports kwenye mechi ya pili.