
Klabu ya Yanga na mshambuliaji Jacques Tuyisenge
Taarifa hizo nyingi zinaenezwa katika mitandao ya kijamii, ambapo kurasa mbalimbali zinatoa taarifa za usajili kuelekea msimu ujao na michango ya klabu hiyo inayoendelea hivi sasa ambazo baadaye ziankuja kukanushwa na uongozi wa klabu.
Jana April 22 klabu ya Yanga imekanusha taarifa mbili zilizosambazwa na page ambazo si rasmi za klabu hiyo katika mitandao ya kijamii. Taarifa ya kwanza ni kuhusu usajili wa mchezaji Jacques Tuyisenge kutoka klabu ya Gor Mahia, ambapo ukurasa huo wa Facebook ambao sio rasmi uliweka picha yake na kuweka maneno "time will tell" yakimaanisha kuwa muda utazungumza.
Taarifa nyingine ya pili ambayo Yanga imeikanusha kupitia ukurasa wake wa Instagram ni ya michango, ambapo taarifa hiyo 'fake' imeeleza kuwa kamati ya michango imekamilisha mkakakati kwa asilimia 100 na kufikisha jumla ya Tsh. Bilioni 2 na kuongeza kuwa imeshapokea barua tatu kutoka kwa matajiri wanaotaka kuwekeza katika klabu hiyo huku kila mmoja akiwa na ofa ya Tsh Bilioni 200.
Yanga imezikanusha taarifa zote na kusisitiza kwa washabiki wake kuendelea kuichangia klabu yao na taarifa rasmi za michango hiyo zitatolewa na kamati husika.
Haijulikani wanaosambaza taarifa hizo potofu wana lengo gani kwakuwa ni tatizo la muda mrefu kwa klabu hiyo. Wengi wanashauri kuwa Yanga iombe uthibitisho rasmi kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii ili kurasa zake ziweze kufahamika na kutofautishwa na kurasa zingine 'fake', kama ilivyofanya klabu ya Simba hivi karibuni kwa kupata 'verification' katika ukurasa wa Instagram na Facebook.