Jumanne , 17th Aug , 2021

Timu ya wananchi Klabu ya Yanga imekamilisha usajili wa wachezaji wote kwenye mfumo wa usajili wa TMS wa Shirikisho la soka Afrika (CAF) na Tanzania (TFF). Amethibitisha Mkurugenzi wa mashindano wa timu hiyo Thabiti Kandoro.

Djuma Shabani, amejiunga na Yanga msimu huu akitokea AS Vital ya Kongo

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo hii leo ikimnukuu Kandoro imethibitisha kukamilisha hatua hizo za usajili wa wachezaji wao wapya waliowasajili kuelekea msimu mpya wa mashindano wa 2021-21.

"Tumekamilisha usajili wa wachezaji wetu wote 28, hii inamaanisha wote wameingia kwenye mfumo wa CAF na TFF, na pia tumeshapata ITC za wachezaji sita kati ya saba na tunaamini baada ya muda si mrefu tutapata ITC iliyobakia, ITC iliyobaki ni ya Khalid Aucho kutoka klabu ya Misr Makassa ya nchini Misri ambapo tunataraji kuipata wakati wowote kuanzia sasa." amesema Kandoro.

ITC (International Transfer Certificate) ni hati ya uhamisho ya kimataifa kwa wachezaji wa mpira ambao uhamisho wao huwa ni wakutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, na hati hiyo hutolewa na Shirikisho sokla la nchi anayotoka mchezaji kwenda kwenye shirikisho la soka la nchi la timu anayojiunga nayo.

Kwa sasa klabu ya Yanga ipo nchini Morocco kwa maandalizi ya msimu ujao wa mashindano (Pre-season) msimu wa 2021-22. Na leo timu hiyo imefanya mazoezi ya kwanza nchini humo ikuwa na kikosi cha wachezaji 28.