Yanga yamgeukia mazima Andrew Vicent 'Dante'

Alhamisi , 10th Oct , 2019

Uongozi wa klabu ya Yanga umesema kuwa mchezaji Andrew Vicent 'Dante' amekiuka masharti ya mkataba kwa kudai maslahi yake  wakati yuko nje ya klabu.

Andrew Vicent 'Dante'

Hayo yamesemwa na Afisa Uhamasishaji na Msemaji wa klabu hiyo, Antonio Nugaz katika mkutano na wanahabari Makao Mkauu ya klabu hiyo, ambapo amesema kuwa Dante anadai malipo yake wakati bado anaendelea kupokea mshahara wa kila mwezi.

"Nimekuwa nikipigiwa simu nyingi sana kuhusu suala la Dante, huwezi kuwa unapokea mshahara halafu haupo eneo la kazi kwa maana kwamba kama hutaki na unataka ile hela kubwa watu wanadai wakiwa kazini. Dante ni mwajiriwa wa Yanga na wala hajaiajiri Yanga", amesema Nugaz.

"Ukitaka kudai malipo yako njoo ufanye kazi halafu kama kile kipindi mlichokubaliana haujalipwa ndio unaweza kutoka na kusema hujatendewa haki lakini sio unalipwa mshahara wa mwezi halafu hutaki kufanya kazi sio sawa", ameongeza.

Pia Nugaz ameongeza kuwa wanaandaa utaratibu wa pamoja na wadhamini wao kuhusu kuwaandalia motisha wachezaji wao endapo watashinda katika mchezo wa nyumbani wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Pyramids ya nchini Misri utakaopigwa Oktoba 27 katika uwanja wa taifa.