Jumamosi , 20th Sep , 2014

Timu ya soka ya Dar es salaam Yanga SC imeanza vibaya ligi kuu ya soka Tanzania bara baaada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 toka kwa wenyeji woa timu ya soka ya Mtibwa Sugar katika mchezo mkali uliopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro

Kikosi cha cha kwanza cha mabingwa wa ngao ya jamii timu ya Dar es salaam Yanga Afrikans.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Dominick Nyamisana wa Dodoma, aliyesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Milambo Tshikungu wa Mbeya, hadi mapumziko tayari Mtibwa Sugar walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0

Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na DC Motema Pembe ya DRC, Mussa Hassan Mgosi kunako dakika ya 17 akimalizia pasi ya kichwa ya Ame Ali na kumuwahi kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyetokea vizuri kutaka kudaka na kumvisha kanzu na mpira kujaa wavuni

Baada ya bao hilo, nyuki wakaingia uwanjani jambo lililosababisha wachezaji walale chini kwa dakika mbili, kabla ya hali kutulia baada ya wadudu hao kuondoka na mchezo huo kuendelea.

Dakika ya 82 mpishi wa bao la kwanza, Ame Ali aliifungia Mtibwa bao la pili baada ya kufanikiwa kuwahadaa mabeki wawili wa kati wa Yanga SC, Nadir Haroub ‘Cannaaro’ na Kevin Yondan kisha kumtungua Dida kufuatia pasi nzuri ya Hassan Ramadhani.

Nao mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Azam fc wao hii leo wameanza vyema mbio za kutetea taji lao, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa ndani ya dimba la Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

Ushindi huo unakua kama kumfuta machozi kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya kufungwa hivi karibuni kushuhudia timu hiyo ikilala kwa bao 3-0 mbele ya Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii

mabao ya Azam FC katika mchezo huo yamepachikwa na mrundi Didier Kvumbangu aliyefunga mawili na moja likifungwa na beki kisiki wa timu hiyo Aggrey Morris
Huku goli pekee la Polisi likifungwa na nahoda Bakari katika dakika ya 60 kwa shuti la umbali wa mita 22

Na matokeo ya michezo mingine ya ligi hiyo ni jijini Mbeya katika dimba la sokoine wenyeji Mbeya city wamebanwa mbavu na maafande wa JKT Ruvu toka Mlandizi mkoani Pwani baada ya kutoka suluhu ya 0-0

Katika uwanja wa mkwakwani jijini Tanga wenyeji wa uwanja huo timu ya JKT Mgambo Shooting waliizamisha timu ya Kagerac Sugar ya Bukoba kwa bao 1-0

katika uwanja wa mabatini Mlandizi mkoani Pwani maafande wa magereza toka Mbeya timu ya Tanzania Prisons wamewachapa wenyeji wao Ruvu Shooting kwa jumla ya mabao 2-0

Na kule katika uwanja wa Kambarage Shinyanga wageni wa ligi hiyo Stand United wamekubali kichapo cha aibu nyumbani mbele ya wageni wenzao timu ya Ndanda FC toka Mtwara baasa ya kuchapwa mabao 4-1

Ligi hiyo itaendelea tena kesho Septemba 21 mwaka huu katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam baina ya Simba na Coastal Union.