Jumanne , 3rd Mei , 2016

Yanga imezidi kuusogelea ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kuafutia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Stand United jioni ya leo Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ukiwa ni moja ya michezo yake minne iliyobakia katika mbio za kuwania utetezi wa kombe.

Washambuliaji wa kimataifa wa Yanga Mzimbabwe, Donald Ngoma kulia na Amissi Tambwe wa Burundi kushoto.

Ushindi huo ulitokana na mabao mawili ya washambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wa Burundi, unaifanya Yanga ifikishe pointi 68 baada ya kucheza mechi 27.

Yanga sasa inaweza kutangaza ubingwa ndani ya mechi mbili zijazo kati ya tatu za mwisho, iwapo itaendeleza wimbi la ushindi.

Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, Yanga tayari walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yote yakifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma.

Ngoma alifunga bao la kwanza dakika ya pili kwa shuti kali, baada ya kuupitia mpira kwenye himaya ya mabeki wa Stand, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Assouman David.
 
Ngoma tena akawainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 45 kwa bao zuri akimlamba chenga kipa wa Stand United, Frank Muwonge baaada ya kutanguliziwa pasi nzuri na Mrundi, Amissi Tambwe.

Kipindi cha pili, Yanga ilikianza vizuri tena na kufanikuwa kupata bao la tatu lililofungwa na Tambwe dakika ya 63 akimalizia kona ya winga Simon Msuva.  

Elias Maguri akaifungia bao la kufutia machozi Stand United dakika ya 82 baada ya kiungo wa Yanga Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kumchezea rafu kiungo wa Stand, Suleiman Kassim 'Selembe.' 

Yanga waliendelea kulisakama lango la Stand, lakini bahati yao leo ilikuwa ni 3-1.

Na kwa upande wa ufungaji sasa Mrundi Amis Tambwe anashika usukani kwa magoli 20 akifuatiwa na Mganda Hamis Kiiza wa Simba mwenye magoli 19.

Yanga wanarejea jijini Dar es Salaam kucheza mchezo wao wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Esperanca ya Angola utakaopigwa Mei 7 katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.