Zahera anavyowapoteza mashabiki wa Yanga

Jumatano , 15th Mei , 2019

Licha ya ushindi mwembamba wa jana dhidi ya Ruvu Shooting, kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ameedelea kubebesha mzigo wa lawama kwa waamuzi na Bodi ya Ligi.

Kocha Mwinyi Zahera (katikati) akisalimiana na Mwenyekiti mpya wa Yanga, Dk Mbette Msolla.

Mara kadhaa, Zahera amekaririwa akiwalaumu waamuzi pamoja na uongozi wa Bodi ya Ligi kuwa wanaikandamiza klabu hiyo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo dhidi ya Ruvu Shooting, na Yanga kuibuka na ushindi mbembamba wa bao 1-0 kupitia kwa Papy Tshishimbi, kocha Zahera amesema, "malalamiko yangu yapo katika pande mbili, kwanza ni kwa upande wa marefa, wapo wanaokuja wakisema kuwa leo Yanga hatoki".

"Namna nyingine ni kwamba kuna mpango katika timu za Simba na Yanga. Sisi tunacheza FA tarehe 6, Azam FC anacheza na sisi tarehe 29, Lipuli na KMC nao wanacheza FA, lakini hakuna mtu ambaye anacheza ligi wakati anatakiwa kucheza nusu fainali ya FA ni Yanga peke yake", ameongeza.

Tuhuma za Zahera za klabu yake kuonewa limekuwa likibebwa kwa nguvu hadi na mashabiki wa klabu hiyo, wakiamini kuwa ubingwa wa msimu huu wataukosa kutokana na figisu za waamuzi na Bodi ya Ligi ambayo wanaituhumu kuipendelea klabu ya Simba.

Mwinyi Zahera amekuwa akionekana kuwa muwazi hadi kupitiliza na wadau wengi wa soka wanakosoa kitendo hicho kwa kuwa kinamharibia taaluma yake kama mwalimu. Wengi wanaamini majukumu yake ni kuzungumzia mafanikio na mapungufu ya kiufundi ya timu yake pamoja na wachezaji wake, badala ya kujihusisha na malalamiko ambayo yanatakiwa kuwasilishwa kwa Bodi ya Ligi kupitia njia sahihi na uongozi wa klabu.

Yanga hivi sasa inaongoza ligi ikiwa na alama 83 baada ya kucheza jumla ya michezo 36, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 82 ambayo imecheza michezo 33.

Bonyeza hapa chini kumsikiliza kocha Zahera.