Ijumaa , 30th Sep , 2022

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anafuatilia na anawatakia mema Timu ya Taifa ya Tembo Warriors ambayo Oktoba Mosi mwaka huu wataingia dimbani kuanza kupambani ubingwa wa Kombe la Dunia

Akizungumza kwa njia ya simu na wachezaji hao kutokea Tanzania kupitia kwa Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi ambaye ametangalia hapa Instanbul kuja kuongeza hamasa, Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania ipo pamoja na wao katika kila hatua na ndio maana Rais ameridhia viongozi wa Wizara kuambatana nao katika fainali hizo.

“Rais na Serikali yenu tupo pamoja na nyinyi, nendeni mkalipiganie Taifa, onesheni uzalendo na kuhakikisha mnarudi na Kombe nchini na hiyo itakuwa ni zawadi kwake Mhe. Rais na Tanzania kwa ujumla”’ amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Aidha ameahidi zawadi nono kwa timu hiyo ikiwemo shilingi milioni 40 endapo watafuzu robo fainali, shilingi milioni 80 wakifuzu kucheza nusu fainali na shilingi milioni 100 wakifanikiwa kufuzu fainali za michuano hiyo.

Ameongeza kuwa yeye mwenyewe baadaye atafika Uturuki na pamoja na kuwapa hamasa hiyo anatarajia kufanya mazungumzo na Waziri wa Michezo na kusaini mkataba wa mashirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika sekta za michezo ili kusaidia kukuza sekta hiyo nchini Tanzania.

Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo Steven Manumbu ameahidi ushindi kwa Mhe. Waziri na kusema kuwa timu ipo tayari kwa ajili ya kuipambania nchi yao.

Naye kocha wa timu hiyo Salvatory Edward amesema morali ya wachezaji hao ipo juu pia wanatambua nini wanatakiwa kufanya na wanashukuru kwa uwezeshaji wote wa Serikali