MBUNGE wa Jimbo la Arsuha Mjini, Godbless Lema,amesitisha maandamano ya kuishinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),kuongeza muda.
Akizungumza leo Arusha na waandishi wa habari, Lema, amesema juzi alipokea ushauri kutoka kwa Jaji Mtungi asitishe maandamano na kuahidi kuja Jijini hapa kufanya kikao na wadau wa vyama vya siasa, pamoja na waandaaji wa zoezi hilo la uandikishaji, ili kuondoa sintofahamu inayoendelea.
Amesema maandamano hayo waliyokuwa wayafanye Juni 25 waliyasitisha kwa barua, baada ya Lema kuongea na Jaji Mtungi, ambaye yeye ni mdau wa jambo hilo, kwa sababu yeye ni mlezi wa vyama vya siasa, ambaye ameniahidi atakuwa Arusha hivi karibuni.
Lema amesema sababu nyingine iliyowafanya waahirishe maandamano hayo ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda,aliyoitoa juzi ya kuongeza siku za kuandikishwa, katika kata za Muriet, Olsunyai,Sokoin One, Sinoni na Moshono, ambapo ziliongezwa siku mbili.
Amesema katika siku za nyongeza, wananchi zaidi ya 7,000 wameandikishwa, huku wengine zaidi ya 30,000 wakiwa bado hawajajiandikishwa, katika kata hizo ambazo zoezi hilo limeisha.
Hata hivyo Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi ili kujua ni lini atawasili, Arusha lakini, amepokea simu na kusema yupo kwenye kikao.
Zoezi hilo Mkoani hapa lilianza katika kata sita ambazo ni Moshono, Terrat, Muriet, Osunyai, Sokoni 1 na Sinoni ambapo kata hizo zilikuwa na jumla ya vituo 55.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd mara baada ya siku saba kuisha zoezi hilo, litaendelea Juni 24 katika Kata ya Sekei, Olasiti, Olomoti, Elerai, Sakina na Unga limited, ambapo kutakuwa na jumla ya vituo 44.
Awamu ya tatu itakuwa katika Kata ya Kimandolu, Baraa, Olorien, Themi, Moivaro, Engutoto na Lemara ambapo kutakuwa na jumla ya vituo 55.
Awamu ya Nne ni Kata ya Levolosi, Daraja Mbili, Ngarenaro, Kaloleni, Sombetini na kata ya kati itakayokuwa na vituo 34.