Jumanne , 25th Mar , 2014

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameivunja rasmi Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa mujibu wa Mamlaka aliyopewa kikatiba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu iliyotolewa leo Rais Kikwete ameivunja tume hiyo tarehe 19 Machi mwaka huu katika tangazo la serikali Namba 81 la tarehe 21 Machi 2014, baada ya Jaji Joseph Warioba kuwasilisha bungeni rasimu ya Katiba.

Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 3, Rais amepewa mamlaka ya kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya rasimu ya Katiba kuwasilishwa Bungeni.

Rais aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katika kwa mujibu wa kifungu cha 5 na 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ambapo tume hiyo ilikusanya maoni na kuandaa rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo tayari imewasilishwa kwenye Bunge Maalum.