Jumapili , 17th Jul , 2016

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto nchini Thobias Andengenye amesema bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu mibovu ambayo inakwamisha magari ya zimamoto yasifike eneo la tukio kwa wakati muafaka.

Kamishna Andengenye ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na East Africa Radio na kusema baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kuwepo kwa barabara mbovu, ujenzi holela wa makazi ya watu, misongamano mikubwa ya magari barabarani na kukosekana kwa njia mbadala ambazo wanaweza kuzitumia kwa dharura.

Amesema tayari jeshi hilo limeanza kushirikiana na wananchi katika kupeana elimu ya kujizuia na majanga mbalimbali na mashuleni kwakuwa ndiko kumeonekana kuwa na tatizo la kuwaka kwa moto mara kwa mara na kusababisha hasara kubwa kwa wanafunzi.

Jeshi hilo linatekeleza mipango yake ya kuweka ofisi za zimamoto kila wilaya ili kuhakikisha wanaendana na maendeleo ya nchi ili kuhakikisha wanasogeza huduma hizo karibu na wananchi.