Jumatano , 12th Apr , 2017

Uongozi wa Uwanja wa CCM Kirumba, kupitia Meneja wa Uwanja Steven E. Shija umetoa taarifa za uharibifu wa Uwanja baada ya mechi kati ya Mbao FC na Simba, iliyopigwa siku ya Jumatatu wiki hii.

Mashabiki Simba

Kwa mujibu wa taarifa yake, mechi hiyo imesababisha uharibifu mkubwa kwenye maeneo ya kuingilia wachezaji, waamuzi na Geti Namba 4 ambapo walikuwa wamekaa mashabiki wa Simba.

Amesema uharibifu huo umetokana na mashabiki wa timu ya Simba SC kupanda juu ya maeneo ya kivuli yaliyojengwa kwenye maeneo yaliyotajwa ( Vyumba vya Kubadilishia Nguo kwa wachezaji, Waamuzi na Geti namba Nne), uharibifu huo unadaiwa kupelekea kushindwa kufunga Milango ya Mbele ambapo ni hatari kwa usalama wa maeneo hayo muhimu.

Taarifa hiyo imesema kuwa uongozi wa uwanja umeishazitaarifu mamlaka husika ili zichukue hatua kwa wanaohusika ili kuhakikisha eneo hilo linatengenezwa mapema kabla ya mechi ya Toto African na Simba SC tarehe 15.04.2017.