Jumanne , 27th Mei , 2014

Wizara ya Afya na ustawi wa jamii nchini Tanzania imewataka wananchi watambue kuwa ugonjwa wa dengue upo na wapuuze taarifa za upotoshaji unaofanywa kupitia mitandao ya kijamii, simu za mikononi na mikusanyiko ya watu kuwa ugonjwa huo haupo.

Msemaji wa wizara ya afya na ustawi wa jamii nchini Tanzania, Nsachris Mwamwaja (katikati), akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo hivi karibuni.

Akizungumza na East Africa Radio Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Nsacris Mwamwaja amesema serikali kwa kushirikiana na wananchi inaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kukabiliana nao
na bado hakuna dawa maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu.

Mwamwaja ameongeza kuwa kwa sasa idadi ya wagonjwa wapya jijini Dar es Salaam ni 24 ambapo kutoka wilaya ya Kindondoni ni 9, Temeke 7 na Ilala 8 na waliolazwa ni 17 katika hospitali za Wilaya hizo.

Nao wakazi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam wamezungumzia kuhusu upotoshwaji huo na kuitaka serikali kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika.