Alhamisi , 15th Nov , 2018

Meneja Mkuu wa timu ya taifa ya Argentina, Jorge Burruchaga amesema anaamini kuwa nyota wa timu hiyo, Lionel Messi atarejea kuichezea nchi yake mwaka ujao.

Lionel Messi

Messi hajaichezea nchi yake tangu kumalizika kwa michuano ya kombe la Dunia, ambapo Argentina ilitolewa katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo dhidi ya Ufaransa.

Burruchaga anaamini, kuwa Messi atarudi katika timu ya Argentina wakati wa kampeni yao ya michuano ya Copa America itakayofanyika nchini Brazil mwaka 2019.

"Hakuna tarehe iliyopangwa sasa kwa kurudi kwa Messi na hatarudi kabla ya mwisho wa mwaka," amesema Burruchaga.

"Lakini haiwezekani kwamba hatakuwa katika timu ya kitaifa tena. Hii ni ya muda mfupi, nina hakika kuwa mwaka ujao, atakuwa tena katika timu ya kitaifa ya Argentina".

Gwiji wa soka nchini Argentina, Diego Maradona pia alitabiri Messi, mwenye umri wa miaka 31 atarudi kikosi hivi karibuni.

"Nadhani hivyo, tutaona, kwa sababu kama haitakuwa hivyo basi tuna shida," alisema Maradona.

Argentina hivi sasa iko chini ya kocha wa muda, Lionel Scaloni baada ya kujiuzulu kocha Jorge Sampaoli ambaye aliongoza timu hiyo katika fainali ya kombe la Dunia nchini Urusi.