
Golikipa wa Yanga, Beno Kakolanya (kushoto) na beki, Kevin Yondani (kulia)
Yondani na Kakolanya walipaswa kuondoka leo kuelekea mjini Shinyanga kuungana na wenzao ambao walitangulia Jumanne, ambapo taarifa zinasema kuwa wachezaji hao wamegoma kusafiri kutokana na kutolipwa mshahara yao ya miezi kadhaa pamoja na fedha ya usajili.
Ikumbukwe Yanga hivi sasa inapitia katika kipindi kigumu kutokana na kuandamwa na mgogoro wa uchaguzi mkuu wa klabu, baada ya hatua ya baadhi ya wanachama na mashabiki kupinga maamuzi ya TFF na Baraza la Michezo (BMT) juu ya taratibu na kanuni za uchaguzi huo ikiwemo hoja ya wagombea.
Yanga imeshawasili mjini Shinyanga Jumanne na tayari imeshaanza mazoezi ikijiandaa kwa mchezo huo wa ligi kuu dhidi ya wenyeji Mwadui FC, utakaopigwa katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga kesho, Alhamisi, 22 Novemba.
Aidha, kuelekea mchezo huo, Yanga itawakosa wachezaji wake wengine baadhi akiwemo Papy Tshishimbi na Juma Mahadhi ambao bado mpaka sasa wapo majeruhi.