Alhamisi , 3rd Jan , 2019

Usiku wa jana umeendelea kuwa mtamu kwa mashabiki wa Manchester United ambao walionekana kukata tamaa tangu mwanzo wa msimu hadi katikati ya mwezi Desemba, mwaka uliopita.

Kocha, Ole Gunnar Solskjaer na wachezaji wake

Ni wazi kuwa kwa sasa huwezi kuwaambia chochote mashabiki wa United juu ya wachezaji wao ambao miezi kadhaa nyuma, wao wenyewe ndiyo walikuwa wakwanza kuwalaumu kutokana na kiwango kibovu uwanjani. Lakini jibu rahisi hapa watakuambia kuwa tatizo ni Mourinho na mifumo yake mibovu na ya kizamani.

Baada ya Mourinho kutimuliwa Desemba 16 kufuatia kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa hasimu wao katika mafanikio nchini Uingereza, Liverpool, muda si muda alitangazwa mchezaji aliyedumu klabuni hapo kwa miaka 11, bingwa wa kutokea 'Super Sub', Ole Gunnar Solskjaer.

Mpaka sasa, Solskjaer ameiongoza United kushinda mechi nne mfululizo za ligi tangu alipokabidhiwa timu, akiweka rekodi kuwa kocha wa pili kufanya hivyo kwenye klabu hiyo baada ya takribani miaka 72 kupita ambapo Sir Matt Busby alipoiongoza United kushinda mechi tano mfululizo za ligi.

Man United imefunga mabao 14 katika mechi hizo nne chini ya Solskjaer, ikiwa imezidiwa na Tottenham Hotspur pekee iliyofunga mabao 15 katika mechi nne za mwisho.

Solsjaer amefanikiwa kuitengeneza Man United yenyewe kuwa kama 'Super Sub' kwa matokeo anayoipatia katika kipindi chake kifupi pamoja na kumtengeneza na kumfufua mshambuliaji Romelo Lukaku kuwa kama 'Super Sub' mwingine. Akiwa amefunga mabao mawili mpaka sasa akitokea benchi kwenye mechi mbili za mwisho.

Bila shaka, iwapo Solskjaer ataendelea hivi na kumaliza nafasi nne za juu katika ligi, atapewa mkataba mrefu wa kuifundisha klabu hiyo ambayo imekuwa ikipata shida kushinda taji la EPL tangu kocha Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013.