Ijumaa , 8th Nov , 2019

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara, amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi wa Serikali, ikiwemo ngazi ya Wilaya na Mikoa, kuzuia wananchi kuonesha mabango yenye kero zao kwa kiongozi mkubwa nchi.

Naibu Waziri Waitara, ametoa kauli hiyo Bungeni wakati akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo, ambaye alihoji juu ya wananchi kuzuiliwa kuonesha mabango yao, wakati wa mkutano wa Rais.

Mbunge Vedastus Mathayo ameuliza kuwa "kwanini viongozi wa ngazi za Wilaya wanazuia mabango ya wananchi yasisomwe mbele ya Rais?".

Akijibu swali hilo Naibu Waziri TAMISEMI Mwita Waitara, amesema kuwa wanachofanya viongozi hao sio maagizo ya TAMISEMI na waache mara moja.

"Ni haki ya wananchi kueleza matatizo yao kwa Rais, kama kuna viongozi wanawazuia wananchi sio maelekezo ya TAMISEMI, kama wanafanya hivyo waache mara moja, pia naelekeza madawati ya kupokea kero yaboreshwe" amesema Waitara