Jumanne , 13th Apr , 2021

Bingwa mtetezi wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, klabu ya Bayern Munich na makamu bingwa wa michuano hiyo, klabu ya PSG wanataraji kuchuana vikali saa 4:00 usiku wa leo Aprili 13,2021 kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa michuano hiyo huku Bayern akiwa ugenini.

Mshambuliaji wa PSG, Neymar Junior (kushoto) na Mshambuliaji wa Bayern Munich, Robert Lewandowski (kulia).

Bayern ana mlima wa kupanda kwani amelazimishwa kichapo cha mabao 3-2 akiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza ambao alicheza bila shujaa wake Robert Lewandowski.

Kuelekea kwenye mchezo huo, imethibitika kuwa nyota huyo ataendelea kukosekana licha ya kuwa ameanza mazoezi mepesi tokea aumie goti lake juma lililopita huku winga wake, Serge Gnabry na kiungo wa kati, Corentin Tolisso wote wakithibitishwa kukosekana.

Kukosekana kwa nyota hao hususani Lewandowski inaaminika kulichangia kwa Bayern kushindwa kuibuka na ushindi kwani walipiga mashuti 31 na kuambulia mabao 2 pekee na mengi yakikosa kulenga lango.

Lewandowski ameshafunga mabao 42 na kutengeneza mabao 8 hadi hivi sasa kwenye michezo 36 aliyocheza kwenye michuano yote na kuchangia mabao 50 kwenye mabao 117 waliyofunga Bayern msimu huu.

Nao, matajiri wa jiji la Paris nchini Ufaransa, klabu ya PSG wanataraji kuingia kifua mbele baada ya ushindi wa mabao mengi ugenini lakini kwa kufurahia Bayern kuendelea kucheza bila Lewandowski na Serge Gnabry.

PSG, wanataraji kumkosa mlinzi wake wa kati, Marquinhos mwenye majeraha ya misuli huku kiungo Marco Veratti na mlinzi wa kulia Alessandro Florenzi akitazamiwa kurejea baada ya kupatwa na Covid-19 majuma yaliyopita.

Wakati Bayern wanatazamiwa kuingia vitani kusaka uwezekano wa kipindua matokeo na kutetea ubingwa wake, lakini rekodi zinaonesha kuwa, Mara ya mwisho Bayern kupindua matokeo ilikuwa mwaka 2014-15 baada ya kuifunga FC Porto na kutinga hatua ya nusu fainali.

PSG anaongoza kumfunga Bayern, kwani amemfunga michezo 6 na Bayern akishinda michezo 4 pekee bila wawili hao kutoa sare kwenye michuano hiyo.