Jumanne , 19th Apr , 2022

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi limetangaza kuendelea na uchunguzi wa kifo cha Padri Francis Kangwa Raia wa Zambia aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mbezi Mshikamano iliyopo Wilaya ya Ubungo, Dar es salaam.

Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro ameeleza kuwa mwili wa Padre Kangwa ulikutwa ndani ya tenki kubwa la maji lililopo nyuma ya nyumba ya makazi ya Mapadri iliyopo mtaa wa Sokoine jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi unaonesha dalili kwamba Padri huyo anaweza kuwa amejiua lakini Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini sababu halisi iliyopelekea kifo cha Padri huyo.

Padri huyo alifika katika kanisa la “St. Joseph” lililopo mtaa wa Sokoine Aprili 12, 2022 kwa ajili ya ibada maalum, na mara baada ya ibada alielekea kwenye makazi ya Mapadri kujipumzisha lakini hakuonekana mpaka Aprili 15, 2022 alipokutwa amefariki katika eneo hilo.