Jumapili , 9th Oct , 2022

Baadhi  ya wakulima wa mazao mbalimbali katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, wameiomba serikali kuongeza idadi ya maafisa ugani vijijini, ili waweze kuwatembelea kwa wakati kuwahamasisha kulima mazao mengine ya biashara, na kuwapatia elimu juu ya matumizi bora ya mbolea.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa kugawa mbolea ya kupandia kwa wananchi yenye ruzuku ya serikali, wakulima hao wamesema kuwa uwepo wa maafisa ugani wa kutosha utawawezesha kulima kwa tija, na kuitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa kuwaletea mbolea hiyo ambayo wananunua mfuko mmoja kwa shilingi 70,000, tofauti na bei za madukani ambapo mfuko mmoja ni kati ya shilingi 140,000 hadi 150,000.
 

"Wakulima tumekuwa tukitumia nguvu nyingi katika kuzalisha lakini tija inakuwa ni ndogo kwa sababu upatikanaji wa pembejeo ni changamoto maana mbolea za madukani zimekuwa na gharama kubwa, lakini kwa mbolea hii ya ruzuku tutapata faida kubwa" wamesema.

Kwa upande wake katibu tawala wa wilaya ya Muleba Greison Mwengu amesema kuwa kwa sasa wamepokea mbolea ya awali ambayo ni tani 10, na kwamba lengo ni kuleta tani 2,628 ambazo ndiyo mahitaji halisi ya wilaya hiyo.
 

"Shime kwa wakulima wote tujitokeze kwa wingi tufike hapa chama cha msingi cha Tukutuku, tununue mifuko ya mbolea kwa gharama nafuu yenye punguzo la serikali" amesema katibu tawala huyo.