Jumatano , 14th Dec , 2022

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wanawake nchini  kujiamini na kutoka mbele kupaza sauti zao ili kukabiliana na wimbi la vitendo vya ukatili vinavyowakabili

Waziri Gwajima amekutana na wananchi wa Kata ya Kirongwe alipotembelea eneo hilo kukagua uundwaji wa Kamati za kupambana na ukatili wa wananwake na watoto wilayani Mafia

Waziri huyo ameonesha kutoridhishwa na uhai Mabaraza ya Watoto na Kamati za MTAKUWWA hasa kwenye ngazi za Vijiji na Kata, ambapo ameahidi kurudi wilayani Mafia na kupiga kambi ili aweze kuwafikia hadi wananchi walio katika visiwa vingine vidogo vidogo vinavyounda wilaya hiyo

Awali, Dkt. Gwajima alipokea taarifa kuwa matukio yanayoongoza kwa wilaya ya Mafia ni; ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na mashambulio ya aibu

Kwa Mwaka 2021/2022 Jumla ya matukio 493 yalitolewa taarifa katika Ofisi za Ustawi wa Jamii na kituo cha Polisi ambapo matukio 56 yalikuwa ya ubakaji na ulawiti, kutelekezwa 64, shambulio la mwili 134 na  shambulio la aibu matukio 239

Kati ya kesi hizo zilizotolewa taarifa, kesi 53 zipo Mahakamani na kesi 4 wahusika wamefungwa ambapo mmoja amefungwa maisha, kesi 5 wapo katika kifungo cha nje, kesi 11 zimekosa ushahidi na kesi 9 zinaendelea.