Jumapili , 26th Feb , 2023

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri zote nchini zinazotekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza usalama wa chakula (LDFS) kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis

Ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya LDFS inayofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora.

Mhe. Khamis amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo ya wananchi katika halmashauri hizo na hivyo ni wajibu wa wasimamizi wa miradi hiyo kutoa kutoka taarifa za hatua mbalimbali za mafanikio na changamoto zilizopo katika miradi ili wananchi ambao ndio wanufaika na walengwa wa miradi hiyo waweze kujulishwa.

“Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa LDFS katika halmashauri tano nchini ambao unagusa maslahi ya wananchi na jamii kwa ujumla, natoa rai kwa wasimamizi wakiwemo viongozi na watendaji wa miradi kuweka utaratibu wa kutoa taarifa za miradi hii kwa wananchi na jamii inayowazunguka” amesema Mhe. Khamis.

Mhe. Khamis amesema Serikali Rais haitaki kuona usiri wa upatikanaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo

Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa LDFS Wilayani Nzega, Mratibu wa mradi Hassan Mtomekela amesema una jumla ya walengwa 672 ambao wamepatiwa mafunzo mbalimbali katika usimamizi wa miradi ya mashamba darasa, utunzaji na uhifadhi wa misitu, uvunaji wa maji ya mvua, ufugaji nyuki.