Ijumaa , 14th Nov , 2025

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali tukio la kuchomwa moto kwa msikiti wa Hajja Hamida katika Ukingo wa Magharibi akieleza kuwa mashambulizi dhidi ya maeneo ya ibada kamwe hayakubaliki.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ramallah imesema walowezi wa Israel wameteketeza moto msikiti wa Hajja Hamida ulioko karibu na mji wa Deir Istiya, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.

Wizara hiyo imeeleza kuwa tukio hilo linakiuka wazi utakatifu wa maeneo ya ibada na linaonyesha ubaguzi uliokita mizizi unaowaongoza walowezi chini ya ulinzi wa serikali ya uvamizi.

Picha za shirika la habari la AFP zimeonyesha nakala za kitabu kitakatifu kwa Waislamu cha Quran zilizochomwa na kuta za msikiti zilichorwa kwa maandishi ya chuki.

Jeshi la Israel limesema vikosi vya usalama vimetumwa katika eneo hilo baada ya kupokea taarifa kuhusu washukiwa walioteketeza msikiti huo, lakini hakuna mtu yeyote aliyekamatwa.

Uchunguzi wa tukio hilo umehamishiwa kwa polisi wa Israel na taasisi za usalama. IDF imelaani tukio hilo na kusema itaendelea kuhakikisha usalama na utulivu katika eneo hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, pia amelaani shambulio hilo kupitia msemaji wake Stephane Dujarric, akieleza kuwa matendo ya vurugu yanayolenga maeneo ya ibada kamwe hayakubaliki.